Rais Dkt. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na kuwahakikishia
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi
ushirikiano kati yake na wafanyakazi
Katika Mazungumzo hayo yaliyofanyika
Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Magufuli amesema pamoja na
kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri
wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha
maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali
inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea
kuchukua hatua za kukabiliana nazo kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.
“Nataka kuwahakikishia
nyinyi viongozi wa TUCTA na wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano inawapenda wafanyakazi na ipo tayari kuwapigania, jambo la msingi
tutangulize maslahi ya Taifa, kawaambieni wafanyakazi wachape kazi na
Serikali itawalinda” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wao Viongozi wa TUCTA
wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Tumaini Nyamhokya
wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na
Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa
watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na
kulipa madeni ya watumishi.
Viongozi hao wameahidi kushirikiana na
Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi na wameomba
Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi
ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi.
0 comments:
POST A COMMENT